Tom Regan: Falsafa ya haki za wanyama - Dibaji ya Marly Winckler

 

Tom Regan: Falsafa ya haki za wanyama

Dibaji ya David Sztybel

Maoni ya mwisho ya Christian Koeder


Dibaji ya Marly Winckler

Kitabu cha Falsafa ya Haki za Wanyama (The Philosophy of Animal Rights), kilichoandikwa na Tom Regan, na kuchapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1989, inaweka katika mfumo na kusambaza kwa lugha iliyo rahisi zaidi hoja kuu aliyoikuza awali katika kitabu chake Hoja ya Kutetea Haki za Wanyama (The Case for Animal Rights (1983), ambacho ni mojawapo ya kazi zilizo makini zaidi, zenye mshikamano mkubwa wa kimantiki, na zenye hoja kubwa zaidi katika maadili ya haki za wanyama. Kazi ya Regan ni sehemu ya mjadala ambao tayari ulikuwa umejengeka, ambapo kuchapishwa kwa Ukombozi wa Wanyama (Animal Liberation) na Peter Singer mwaka 1975 kulikuwa hatua muhimu sana ya kihistoria. Hivyo basi, Hoja ya Kutetea Haki za Wanyama (The Case for Animal Rights) pamoja na muhtasari wake wa baadaye vilijitokeza katika wakati ambao uwezo wa wanyama kuhisi (animal sentience), tatizo la mateso, na ukosoaji wa ubaguzi wa spishi (speciesism) tayari vilikuwa vimejengeka kwa kiwango kikubwa ndani ya uwanja wa falsafa.

Regan anapiga hatua moja mbele zaidi kwa kuunda nadharia ya haki za wanyama inayojengwa juu ya dhana ya thamani ya asili (inherent value) na wazo la “wahusika wa maisha” (subjects-of-a-life). Mtazamo huu hauishii tu kukosoa vitendo vya ukatili wa hali ya juu dhidi ya wanyama, bali pia unahoji uhalali wa kimaadili wa unyonyaji wa wanyama wenyewe. Kwa msingi huo, unakataa aina yoyote ya matendo yanayowafanya viumbe hawa kuwa bidhaa za kufanikisha malengo ya binadamu, badala ya kuwatambua kama viumbe wenye thamani yao ya ndani inayostahili kuheshimiwa.

Hata hivyo, zaidi ya miongo mitatu baada ya kuchapishwa kwa kitabu hiki—na miaka hamsini tangu kuchapishwa kwa Ukombozi wa Wanyama (Animal Liberation)—tunakabiliwa na mkinzano wa kihistoria unaotia wasiwasi: kamwe hakujawahi kuzalishwa maarifa mengi kiasi hiki ya kisayansi na kifalsafa katika nyanja ya maadili ya wanyama, na wakati huohuo kamwe hakujawahi kuwepo idadi kubwa kiasi hiki ya wanyama wanao nyanyaswa kwa kiwango kikubwa katika viwanda/mashamba ya ufugaji kama ilivyo leo. Uwazi na maendeleo ya kinadharia yameongezeka kwa kiwango cha ajabu; hata hivyo, mwamko wa kijamii na mifumo ya kisiasa imeendelea kubaki nyuma kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na maendeleo hayo.

Tangu miaka ya 1970, hoja madhubuti zimeweka msingi imara wa kuthibitisha kwamba wanyama wana uwezo wa kuhisi (animal sentience), zimebomoa hoja za ubaguzi wa spishi (speciesism), na zimeonyesha wazi kutokuwiana kwa kimaadili kwa mifumo inayowafanya viumbe wenye hisia kuwa bidhaa za kutimiza malengo ya binadamu. Katika kiwango cha kimaarifa na kifalsafa, uhalali wa kimaadili wa unyanyasaji wa wanyama umeterereshwa kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo, mapinduzi haya ya kimawazo hayajatafsiriwa kuwa mabadiliko ya kimuundo katika jamii.

Umma kwa ujumla, ingawa sasa ina taarifa na uelewa zaidi kuhusu masuala ya haki za wanyama, bado kwa kiasi kikubwa imeendelea kuishi ndani ya mifumo ya kitamaduni na ulaji inayotegemea unyanyasaji wa wanyama. Hali hiyo pia inaonekana pia miongoni mwa wasomi na viongozi wa kisiasa, kiuchumi, kisanii na kidini, ambao kwa sehemu kubwa wameendelea kudumisha desturi zao, mitazamo yao na mahusiano yao ya awali bila mabadiliko makubwa. Mateso ya wanyama sasa yanaonekana zaidi na yanajulikana kwa watu wengi, lakini bado hayajawa kipaumbele; yamefahamika zaidi, lakini hayajawa sehemu ya msingi ya maamuzi na mijadala ya kijamii.

Pengo hili linaweza kuelezwa kwa kiasi fulani na kuendelea kuwepo kwa ukosefu wa elimu ya maadili kuhusu haki za wanyama, ambayo bado ni nadra sana hata katika taasisi za elimu ya juu. Wanafunzi katika vyuo vikuu na vyuo vya kati mara chache hupata mafunzo ya kina na ufahamu mbadala kuhusu maadili ya wanyama au haki haki zao zinazojengwa katika misingi ya hoja. Kwa wale wanaomaliza programu hizo—au ambao hawapati kabisa elimu ya baada ya sekondari—masuala haya hubaki mbali zaidi na uelewa wao. Nje ya duru maalumu za kitaaluma na za wanaharakati, hoja zinazojengwa juu ya haki za wanyama kwa kiasi kikubwa hazipo katika vyombo vikuu vya habari na mijadala ya umma. Hata hivyo, pengo hili linaonekana kwa nguvu zaidi katika ngazi za taasisi za kisiasa, ambapo, katika nchi nyingi mabunge na taasisi za kutunga sheria huathiriwa kwa kiasi kikubwa—na mara nyingi hata kudhibitiwa—na makundi yenye nguvu ya maslahi ya kiuchumi, hasa sekta ya biashara kilimo (agribusiness) na mfumo mpana wa viwanda kilimo na mifugo (agro-industrial complex). Sekta ambazo uhai wake wa kiuchumi unategemea moja kwa moja ukandamizaji wa wanyama na huwa na ushawishi mkubwa katika uchaguzi, uundaji wa ajenda za mabunge, na sera za umma, hali ambayo huendeleza na kuimarisha pengo kati ya mwamko wa kimaadili na mabadiliko halisi ya kimuundo katika jamii.

Mpangilio huu umegeuza mjadala kuhusu haki za wanyama kuwa eneo ambalo karibu ni mwiko kulijadili, ambapo mapendekezo ya kimaadili hukinzana moja kwa moja na maslahi ya kiuchumi yaliyokita mizizi, na hivyo kusababisha maendeleo ya polepole na yasiyoendelevu. Hata mipango kama Jumatatu Isiyo na Nyama (Meatless Monday), inayohimiza kupunguza matumizi ya bidhaa zinazotokana na wanyama, hukumbwa na upinzani mkali usioendana na ukubwa wa pendekezo lenyewe, hasa kwa sababu ya umuhimu wake wa kiishara na kielimu. Upinzani huu hauwezi kuelezwa kwa athari za haraka za kimatendo za mpango huo, bali unatokana na ukweli kwamba, hata kama ni kwa siku moja tu, unavunja mtazamo wa kuuchukulia ukandamizaji wa wanyama kuwa jambo la kawaida na lisilohojiwa, huku ukionyesha uwezekano halisi wa mifumo mbadala ya lishe na utamaduni.

Mtindo huu wa mwitikio na upinzani unadhiirisha ukweli mmoja muhimu: maendeleo ya kimaadili katika nyanja ya haki za wanyama bado yanategemea zaidi duru maalumu za kihistoria zinazofungua fursa za mabadiliko kuliko uwepo wa mifumo ya kudumu ya haki. Duru hizi za kipekee zinapofungwa, hali ya kurudi nyuma au kusimama kwa maendeleo huwa ndiyo inayotawala. Kile ambacho kingepaswa kuwa sera endelevu ya umma mara nyingi hugeuka kuwa tukio la muda mfupi tu, na kile ambacho kingepaswa kutambuliwa kama haki ya msingi mara nyingi hubaki kuwa hatua ya mpito inayoweza kuondolewa wakati wowote.

Hapa ndipo mvutano unapoibuka ambao hatuwezi kuuepuka. Tom Regan yuko sahihi katika uchunguzi wake wa maadili; hata hivyo, uzoefu wa kihistoria unaonyesha kwamba kudai kila kitu kama sharti la kuchukua hatua mara nyingi husababisha kusonga mbele kidogo sana—au kutokusonga kabisa. Juu ya hili kunaongezwa jambo linalojirudia katika harakati za kisiasa na kimaadili: ukosoaji wa ndani usioelekezwa kwa wapinzani wa nje, ila kwa mipango ya mpito inayotoka ndani ya uwanja wa haki za wanyama wenyewe. Mbali na kuimarisha sababu ya utetezi wa wanyama, mienendo kama hiyo huwa inagawanya hata zaidi harakati dhaifu ya kisiasa, ikibadilisha muunganiko unaowezekana kuwa mgongano wa ndani, kudhoofisha uwezo wa kuchukua hatua za pamoja, na kupoteza fursa muhimu za kujenga msingi wa pamoja wa kuwasaidia wanyama kwa ufanisi.

Kwa kuzingatia hili, swali linakuwa lisiloepukika: je, tunapaswa kujiepusha na kuchukua hatua kwa sababu tu hatuwezi kufikia kila kitu kwa wakati mmoja? Kwa Regan, mageuzi ya taratibu huwa yanaongeza muda wa ukosefu wa haki kwa kuhalalisha miundo ambayo inapaswa kufutwa. Hata hivyo, uzoefu wa kihistoria unaonyesha kuwa kusimamisha au kukana uhalali wa hatua zinazofaa, zinazopimika na zenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya kisiasa kwa jina la usafi wa dhana bora  kunamaanisha, kwa vitendo, kukubali kuendelea kikamilifu kwa madhara yale yale yanayodaiwa kupingwa.

Kudumisha lengo la kutokomeza kabisa matumizi na ukandamizaji wa wanyama kama dira ya kimaadili ni jambo la msingi. Lakini kuichukulia dira hiyo na sharti la kuchukua hatua za mara moja kunaweza kubadili uthabiti wa kimaadili na kuwa kupooza kisiasa. Kati ya kuukubali udhalimu kama ulivyo na kudai ukomeshwe mara moja, kuna njia ya kati. Katika njia hiyo—ambayo si kamilifu, inayopingwa, na inayofanyika hatua kwa hatua—watu hubadilisha tabia zao, na namna wanavyowaona kuwatendea wanyama huanza kubadilika. Njia hii haipunguzi uzito wa dhuluma ya ukandamizaji wa wanyama; inatambua tu kuwa hoja sahihi ya kimaadili haitafsiriwi moja kwa moja kuwa mabadiliko ya kihistoria. Mabadiliko ya aina hii hutegemea mapambano halisi ya kisiasa. Kudharau nafasi hii ya mpito hakuharakishi ukombozi wa wanyama; bali kunadumisha tu hali iliyopo.

Kila mlo usio na bidhaa zinazotokana na wanyama unaotolewa katika shule za umma si ishara ndogo isiyo na maana. Ni uzoefu halisi unaofundisha ladha mpya, unaofanya mbadala kuwa jambo la kawaida, unaobadilisha marejeo ya kitamaduni, na kupanua upeo wa kile kinachoonekana kuwa kinawezekana. Hili halichukui nafasi ya kutokomeza ukandamizaji wa wanyama, bali huandaa mazingira ambayo yataufanya utokomezaji huo usionekane tena kama jambo lisilowezekana kufikiriwa. Kukataa hatua za mpito zinazofanya kazi kwa jina la njia bora ya kinadharia kunamaanisha kuwanyima msaada wa moja kwa moja wanyama wanaoteseka sasa hivi—msimamo ambao kwa kawaida tusingeukubali kama ungehusu dhuluma dhidi ya binadamu. Viwango hivi viwili vya maadili vinaonyesha uwepo wa upendeleo wa kibaguzi dhidi ya spishi nyingine na kujitenga na hali halisi wanayoishi wanyama wenyewe.

Kitabu cha Tom Regan kinaendelea kuwa mwongozo muhimu wa kimaadili kwa sababu kinaweka wazi kwamba ukandamizaji wa wanyama ni dhuluma inayopaswa kutokomezwa, si kurekebishwa tu. Katika dhana ya maadili, uchambuzi wake hauna utata; lakini katika dhana ya kihistoria na kisiasa, uwazi wa dira ya maadili hautafsiriwi moja kwa moja kuwa mabadiliko ya kijamii. Kati ya kuthibitisha kanuni na kubadilisha kwa vitendo mifumo ya kijamii, ni lazima kujenga madaraja, hata kama ni ya muda na yasiyo kamilifu. Kukataa kujenga hatua hizi za mpito kwa jina la uthabiti wa maadili kunaweza kulinda ubora wa hoja za kimaadili, lakini hakubadilishi sera za umma, hakubadilishi desturi za kijamii, wala hakupunguzi mateso ya kweli na ya haraka ya mabilioni ya wanyama.

Marly Winckler
Florianópolis, Brazil
Januari 2026




Swahili   Kiswahili