Tom Regan: Falsafa ya haki za wanyama - Maoni ya mwisho ya Christian Koeder

 

Tom Regan: Falsafa ya haki za wanyama

Dibaji ya David Sztybel

Dibaji ya Marly Winckler


Maoni ya mwisho ya Christian Koeder

Haki za wanyama

Kwangu binafsi, mtazamo wa Regan unaojengwa juu ya haki ni muhimu sana. Haki za kimaadili (mawazo na kanuni za maadili) pamoja na haki za kisheria (zinazolindwa na sheria) hujenga uzio wa ulinzi unaomzunguka kila mtu binafsi. Wengine hawaruhusiwi kubomoa uzio huo, bila kujali mtu huyo amefanya nini—kama Regan anavyoeleza katika kitabu chake Empty Cages. Fikiria mtu mwovu zaidi unayeweza kumfikiria (kwa mfano, Hitler). Kwa mujibu wa haki za binadamu, ingekuwa ni kosa kumuua. Ndiyo, angepaswa kufungwa gerezani maisha yake yote ili kulinda usalama wa wengine. Wazo la haki za binadamu—lililoimarishwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia, angalau katika nadharia na mara nyingi pia katika vitendo—ni msingi muhimu kwa uhai wa ustaarabu wa kisasa. Ninaposema ustaarabu, ninamaanisha kuishi pamoja kwa amani na kuheshimu kanuni za kidemokrasia: mijadala, sawa; kutokubaliana, sawa; lakini utekaji nyara, mateso, utumwa, mauaji ya kiholela, mauaji ya kulipa kisasi, na hukumu za kifo—haya yote: hapana.

Wazo la haki za wanyama, kwa maana kwamba linakataa aina zote za kuchinja wanyama na linadai ulaji wa mboga (vegetarianism) si kama ni tendo la huruma kwa mtu binafsi pekee bali pia ni dai la kisiasa, limejengwa juu ya msingi wa haki za binadamu. Kwa maana, haki za wanyama zinajumuisha haki za binadamu.

Kuna mitazamo mingine pia inayohusiana na haki za wanyama ambayo inasisitiza kuwaheshimu wanyama na ulaji wa mboga. Mimi binafsi naiona kuwa haina manufaa makubwa. Kwa mfano, dhana ya ukombozi wa wanyama (animal liberation) inalenga kuonyesha kwamba tunapaswa kupinga ukandamizaji na unyanyasaji wa wanyama—si kwamba (kama rafiki yangu mmoja alivyodhani kwa hofu) tunapaswa kufungua mabanda yote ya bustani za wanyama na kuwaacha simba na mamba washambulie watu. Badala yake, “Ukombozi wa wanyama” ni wazo linalolenga mabadiliko ya kijamii.

Aidha, mtazamo wa nadharia ya utumizi (utilitarianism) ya Peter Singer, uliowasilishwa katika kitabu chake Ukombozi wa Wanyama (Animal Liberation), unaruhusu baadhi aina za unyanyasaji wa wanyama ikiwa unyanyasaji huo utazalisha manufaa kwa idadi kubwa ya wengine. Hili linapingana na dhana ya haki za wanyama. Vivyo hivyo, wazo la kupinga ubaguzi wa spishi (speciesism), ubaguzi wa wanyama, kwa sababu ni aina ya dhuluma ni lenye mantiki. Hata hivyo, halitoshi kwani binadamu au mnyama anaweza kutendewa vibaya, ikiwa hakuna mwenye haki.

Safari kuelekea yasiyojulikana?

Ikiwa umeona hoja za Regan zinashawishi na umeamua kuunga mkono haki za wanyama, hatua inayofuata kwa mantiki ni kuwa mlaji wa mboga (vegetarian), au kwa usahihi zaidi, kuwa mvegani (vegan). Kama watetezi wa haki za wanyama na walaji wa mboga, tunaingia katika eneo la kipekee. Msingi wetu ni imara. Tunaweza kuwa na uhakika kwamba lishe ya mboga inaweza kuwa yenye afya na salama. Hata hivyo, tunatembea katika mipaka ya eneo ambalo limechunguzwa kikamilifu, na wakati mwingine tunaingia katika eneo ambalo bado halijulikani. Hadi sasa, hakuna nchi duniani ambayo ni ya walaji wa mboga pekee au ya wavegani pekee. Haki za wanyama zina ushawishi mkubwa wa kimaadili (kwa watu wengi). Pia zinawezekana kutekelezwa kisheria, lakini hilo linawezekana tu ikiwa watu wengi wataafikiana nasi. Kwa hiyo, tunazungumzia mawazo ya kufikirika (utopia) yanayoweza kutekelezeka; tunajua namna ya kuijenga, lakini bado ni maono ya siku zijazo.

Ili kubadili mahali tunakoweza kufika, ni lazima kwanza tutambue tulipo sasa. Ni kana kwamba tunaingia katika eneo lisilojulikana au “msitu” . Safari hiyo inaweza kuwa ya hatari. Kwa nini? Kwa sababu mabadiliko ya kijamii huambatana na hatari pamoja na matokeo yasiyotarajiwa. Hili si tatizo linaloihusu tu harakati za vegan au haki za wanyama. Ni somo la kusikitisha tulilojifunza kutokana na mapambano ya haki za kiraia na haki za wanawake.

Hata hivyo, harakati za haki za wanyama zina upekee wake. Isipokuwa baadhi ya dini zenye kanuni maalumu za lishe, hii ndiyo harakati ya kwanza ya kijamii inayodai kwamba watu wabadili mfumo wao wa ulaji. Muhimu zaidi, kwa miongo mingi sasa, mamilioni ya watu tayari wameingia katika eneo hili “lisilojulikana” la maisha ya vegani. Zaidi ya hayo, eneo hili la vegani limeendelea kupanuka polepole na kuingia katika maeneo ambayo hapo awali yalitawaliwa na ulaji wa vyakula vya bidhaa za nyama.

Hata hivyo, makosa mengi yamefanyika, na mafunzo mengi yamepatikana kutokana na uzoefu huo. Kwa nini tusitumie “maarifa ya ndani” hayo ili kufanya safari yetu iwe rahisi na yenye mafanikio zaidi? Inasemekana, na nami nakubaliana na hilo, kwamba kuna maeneo mawili makuu ambayo mara nyingi husababisha changamoto: (1) lishe na (2) maisha ya kijamii.

Lishe

Vitabu vya mwanzo vilivyounganisha dhana za haki za wanyama na ulaji wa mboga vilianza kuchapishwa mwishoni mwa miaka 1800, hasa kitabu cha Henry Salt, Haki za Wanyama (Animals’ Rights), kilichochapishwa mwaka 1892. Wakati huo, sayansi ya lishe haikuepo. Vitamini, ambavyo ni muhimu kwa afya ya binadamu, viligunduliwa katika nusu ya kwanza ya miaka ya 1900. Shirika la kwanza lililojitambulisha rasmi kama la vegani, yaani The Vegan Society nchini Uingereza, lilianzishwa mwaka 1944. Vitamini ya mwisho kugunduliwa—vitamini B12—ilitengwa na kutambuliwa takriban miaka minne baadaye. Hata hivyo, mawazo mengi kuhusu lishe yaliyopatikana katika vitabu vya kale vya wavegani vya karne ya kumi na tisa yameendelea kurudiwa ndani ya harakati za wavegani hadi leo.

Wakati huo huo, sayansi ya lishe imegundua changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika lishe ya vegan pamoja na njia za kuzitatua. Hivyo basi, tuyatumie maarifa hayo ya kisayansi.

Kama mtaalamu wa sayansi ya lishe na mtu ambaye ameishi maisha ya vegan kwa muda mrefu, ninapendekeza kanuni zifuatazo. Tunaweza kuziita kanuni sita za dhahabu za lishe ya vegan:

  1. Badala ya bidhaa za wanyama, tumia mikunde na vyakula vya mikunde, kama vile tofu, maziwa ya soya, maharage, dengu (ades), kabuli na karanga.
    • Mikunde ni chanzo bora cha protini, madini ya chuma (iron), na zinki.
  2. Tumia kirutubisho cha vitamini B12, isipokuwa kama unatumia vyakula vilivyoongezwa vitamini B12 karibu kila siku.
    • Tumia takribani mikrogramu (µg) 10–50 kwa siku, au µg 2,000 mara moja kwa wiki.
  3. Hakikisha unapata vitamini D ya kutosha, kupitia kirutubisho (takribani µg 20–25 kwa siku) au kwa kupata mwanga wa jua wa kutosha.
  4. Pata iodini ya kutosha kupitia chumvi yenye iodini, mwani wa baharini (kama nori au wakame), au kirutubisho chenye µg 100–150 kwa siku.
  5. Jaribu kutumia mara kwa mara vyakula vyenye asidi mafuta ya omega-3, kama vile mafuta ya mbegu za kitani (flaxseed oil), mafuta ya canola (rapeseed/canola oil), jozi (walnuts), au mbegu za katani (hempseeds).
  6. Kula vyakula vyenye kalsiamu kwa kila siku, kama vile vyakula vilivyoongezwa kalsiamu, sukuma wiki, kabichi ya Napa (kabeji ya kichina, chainizi, napa cabbage), bok choy, au broccoli.

Maelezo ya ziada

  • Kirutubisho cha vegan chenye virutubisho vingi (vegan multinutrient supplement) kinaweza kuwa chaguo rahisi kwa sababu mara nyingi huwa na vitamini B12, vitamini D na iodini kwa pamoja.
  • Vitamini B12 ndiyo kirutubisho muhimu zaidi. Hata watu wanaokula mboga pamoja na maziwa na mayai (ovo-lacto vegetarians) mara nyingi wanashauriwa kutumia kirutubisho cha B12.
  • Lishe bora inapaswa kujumuisha matunda mengi, mboga mbalimbali, nafaka zisizokobolewa (whole grains), mikunde, pamoja na karanga, mbegu na mafuta yenye afya yatokanayo na mimea.
  • Maelezo zaidi kuhusu lishe ya vegan yanapatikana kupitia International Vegetarian Union (IVU) na The Vegan Society.

(2) Maisha ya kijamii

Wakati Donald Watson—mtu aliyebuni neno “vegan”—aliulizwa, “Ni jambo gani unaloliona kuwa gumu zaidi kuhusu kuwa vegan?” alijibu: “Nadhani ni upande wa maisha ya kijamii.”

Unapokuwa mlaji wa mboga (vegetarian), na hasa mvegani, unaweza kukutana na changamoto kutoka kwa watu wanaokula bidhaa za wanyama (omnivores) pamoja na kutoka kwa baadhi ya vegans wenyewe. Baadhi ya walaji wa bidhaa za wanyama watakuunga mkono. Lakini wengine wanaweza kukasirikia, kuhisi kuudhiwa, kukerwa, au kujitetea kana kwamba uchaguzi wako unawakosoa wao. Wengine wanaweza hata kujaribu kuhusisha kila tatizo dogo la kiafya unalopata na lishe yako ya vegan.

Mnamo mwaka 1944, Donald Watson aliandika:

“Tunaweza kuwa na uhakika kwamba, ikiwa hata chunusi moja tu itatokea na kuharibu uzuri wa mwili wetu, dunia itaamini kwamba hilo limetokana kabisa na kosa letu wenyewe kwa kutokula ‘chakula sahihi’.”

Kukutana na wavegani na watetezi wa haki za wanyama kunaweza kuwa jambo la kufurahisha sana. Wanaweza kubadilishana uzoefu, kutoa ushauri, kukutia moyo, na mara nyingi ni watu wenye utu mzuri. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba hili ni kundi lenye watu wa aina mbalimbali. Huenda ukakutana na baadhi ya wavegani ambao mitazamo yao au tabia zao utaziona kuwa za “kipekee” (kama wanavyosema nchini Uingereza) au hata “zisizopendeza” (kama tunavyosema nchini Ujerumani).

Kwa asili, wanadamu si rahisi kuelewana nao kila wakati. Na kuwa mvegani au mtetezi wa haki za wanyama kunaweza kufanya mahusiano ya kijamii yawe magumu zaidi. Hata hivyo, kufuata kanuni chache za msingi kunaweza kurahisisha maisha. Tunaweza kuziita kanuni nne za msingi za kudumisha afya njema ya akili:

  1. Usihubiri. Mamilioni ya wavegani wamejaribu kufanya hivyo bila mafanikio makubwa. Badala yake, fundisha kwa mfano wa maisha yako. Jitahidi kuwa mvegani mwenye furaha, na tumia uanaharakati wa kirafiki (friendly activism). Epuka uanaharakati wa kulazimisha au wenye shinikizo (pushy activism).
  2. Tambua mipaka yako. Omba watu wakuheshimu, nawe pia waheshimu wengine. Kubaliana kwamba watu wanaweza kuwa na mitazamo tofauti. Kusingekuwa na maana ya uvumilivu kama mambo yangekuwa rahisi.
  3. Jumuika na wavegani wengine. Mara nyingi wanaweza kukupa msaada na ushauri muhimu. Hata hivyo, usitarajie wawe wakamilifu au kana kwamba ni jini wa kwenye chupa anayetimiliza kila unachotamani
  4. Tunza afya yako. Usiwe mshupavu wa kupindukia (fanatic). Hakuna jambo lolote maishani linaloweza kufanywa kwa ukamilifu wa asilimia 100.

Hitimisho ni nini?

Kwa upande wa lishe, lishe ya vegan inaweza kuwa yenye afya sana, lakini bila shaka kuwa vegan hakumaanishi moja kwa moja kwamba lishe yako ni bora kiafya. Mambo muhimu zaidi ni kuhakikisha unapata virutubisho muhimu, hasa vitamini B12, na kwamba, kadiri inavyowezekana, msingi wa lishe yako uwe vyakula vya asili ambavyo havijasindikwa sana (whole foods). Swali ambalo limekuwepo kwa karne nyingi na bado hujitokeza mara kwa mara ni: “Je, kimaumbile binadamu ni walaji wa vyakula vya mimea na nyama (omnivores)?” Hata hivyo, kwa mtazamo wa epidemiolojia ya kisasa ya lishe (yaani tafiti za lishe zinazofanywa kwa binadamu) swali hilo si muhimu sana. Aidha, ni swali linalorahisisha mno jambo lenyewe. Swali muhimu zaidi ni: Tafiti zinazowahusu watu wanaofuata lishe ya vegan zinaonyesha nini? Jibu ni kwamba zinaonyesha kuwa lishe ya vegan inaweza kuwa yenye afya sana.

Kwa upande wa maisha ya kijamii, katika historia yote haijawahi kuwa rahisi, yenye urahisi, na inayokubalika zaidi kijamii kuwa mvegani. Kwa maoni yangu, inaweza kuwa mkakati wenye manufaa kukubali kile ninachokiita “mkinzano wa kimaadili” (ethical paradox). Kwa upande mmoja, mtu anaweza kutetea haki za wanyama, kutambua kwamba haki hizo zinadai ulaji wa mboga, na kwamba ulaji wa mboga ulio thabiti kabisa unamaanisha kuwa mvegani. Kwa upande mwingine, unaweza pia kushikilia mtazamo kwamba kila mtu ana haki ya kuchagua aina ya lishe anayopendelea. Kwa mantiki ya kawaida, msimamo huu unaweza kuonekana kuwa na mkanganyiko. Unaweza kuonekana kama mtu anayedai haki za wanyama kama suala la kisiasa, lakini wakati huo huo anavumilia kwa ukarimu ukiukwaji wa haki hizo. Hata hivyo, huu ni mkakati unaoweza kuwasaidia walaji wa bidhaa za wanyama (omnivores) kuvumilia na kukubali mitazamo yako. Hali hiyo inaweza kurahisisha maisha yako na kukusaidia (kwa kutumia maneno ya Colleen Patrick-Goudreau) kuwa “vegan mwenye furaha” (joyful vegan). Zaidi ya hayo, mkakati huu unaweza pia kuwasaidia wanyama, kwa sababu unajenga madaraja yanayoelekea kwenye kutambuliwa kwa haki za wanyama badala ya kujenga kuta zinazowatenganisha watu.

Binafsi, ninapendelea mtazamo huu. Sipendi mitazamo ya kimadhehebu, ya kujinyima kupita kiasi, ya kujitesa, ya kufanya kazi bila kupumzika, au ya kujiona kama shahidi. Kwa kutumia maneno ya Mephistopheles, mhusika katika tamthilia Faust ya Johann Wolfgang von Goethe ya mwanzoni mwa karne ya kumi na tisa: “Mtu hahitaji kujitesa kwa wasiwasi uliopitiliza.” Cha kufurahisha ni kwamba maneno haya yanatamkwa na Mephistopheles, mhusika anayewakilisha aina ya pepo au roho ya ubatili/ukana-maana (nihilism). Ikiwa hupendezwi na ushauri wa pepo, basi unaweza kufuata ushauri wa Donald Watson. Alipokuwa na umri wa miaka 94, alipoulizwa kuhusu mafanikio yake maishani, alisema: “Mimi ni mtu ninayependa kufurahia maisha, mradi tu sifanyi madhara kwangu mwenyewe, kwa watu wengine, kwa wanyama, au kwa sayari yetu.”

Dkt. Christian Koeder
Ellwangen, Ujerumani
Februari 2026




Swahili   Kiswahili