Tom Regan: Falsafa ya haki za wanyama
Maoni ya mwisho ya Christian Koeder
Dibaji ya David Sztybel
Nimekuwa mvegani na mwanaharakati wa haki za wanyama kwa takribani
miaka 37. Nilikuwa na bahati kwamba elimu yangu ya chuo kikuu ilijumuisha
masomo ya kazi za Tom Regan. Baadaye, kazi hizo nilizifanyia utafiti wa kina katika
tasnifu yangu ya shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Toronto iliyoitwa “Empathy and Rationality in Ethics”
(Huruma na Umantiki katika Maadili). Pia nilipata heshima ya kumsikiliza
Profesa Regan akitoa mihadhara katika makongamano mbalimbali. Kama ilivyo kwa
maandishi yake, kila mara nilipata hisia dhahiri kwamba nilikuwa nikijifunza
kutoka kwa mmoja wa wanafalsafa wakubwa kabisa. Ubora wa hali ya juu wa uandishi
unaopatikana katika kitini hiki pia unaonekana na kustawi katika vitabu vyake
vingi vya kifalsafa, ambapo kazi yake maarufu zaidi ni The Case for Animal Rights (Hoja
ya Kutetea Haki za Wanyama).
Ninaiheshimu sana kazi yake, lakini pia naihoji, kwa kufuata utamaduni wa
falsafa ambao unasisitiza uchambuzi na ukosoaji.
Kitabu hicho kinajikita katika mrengo wanadharia ya kuelezea juu ya haki
za mtu binafsi, lakini kinavunja desturi ya muda mrefu iliyokuwa ikichukulia
kwa uzito haki za binadamu pekee. Hata hivyo, yeyote anayewachukulia wanyama
kwa uzito hawezi kushindwa kuona uzito wa hoja za Regan kuhusu haki za mtu
binafsi zinazopatikana pia katika kitini hiki. Regan anasisitiza kwamba maisha
ya wanyama yana thamani/umuhimu kwa wao wenyewe, bila kujali manufaa yao ya
matumizi kwa wanadamu. Anasema kuwa wanyama wana thamani ya asili na
inayojitegemea. Na kwamba wao si bidhaa au rasilimal. Kama anavyoeleza Dk.
Regan, kile kinachowatokea wanyama kina umuhimu kwao wenyewe. Aidha, kila
mnyama kwa usawa ana maisha ambayo yanaweza kuwa mazuri au mabaya kwake,
na kwa sababu hiyo anastahili haki sawa. Kwa msingi huo, Regan
anapendekeza kwamba kanuni za haki zipanuliwe ili kuwajumuisha pia wanyama, na
kwamba wapewe haki yao ya msingi ya kuheshimiwa – haki ambayo ndiyo msingi wa
chimbuko la haki nyingine zote. Msisitizo huu juu ya haki za mtu binafsi bado
una umuhimu wa kipekee katika historia na muhimu wake haujapungua, licha ya
kuongezeka kwa mitazamo ya kudharau hata haki
za binadamu, inaonekana kuongezeka katika masuala mbalimbali ya kimataifa.
Mbali na utetezi wake wa haki za mtu binafsi kwa wanyama, ambao Regan
anautetea kwa nguvu na kwa namna ya kukumbukwa, kitini hiki pia kina kile
ninachokiita “mawazo yanayostahili kusikika tena na tena” (echoables).
Haya ni mawazo na dhamira zinazogusa kwa
kina watu wanaochukulia haki na heshima kwa uzito. Ni hoja ambazo Regan
alizisisitiza na zinapaswa kuwafanya watu wote kutafakari kwa kina. Wanawake na
watu weusi hawapo ili kuwatumikia watu wengine; vivyo hivyo, wanyama hawapo kwa
ajili ya kuwatumikia wanadamu. Hakuna mtu mwenye misingi ya kimaadili
anayefurahia ubaguzi wa kiholela, chuki zisizo na msingi wa haki, au ubinafsi.
Mawazo haya yanagusa mioyo ya wale wote wanaotambua kwamba, hasa katika nyakati
hizi ngumu baada ya kifo cha Regan mwaka 2017, tuna wajibu wa kutokukata tamaa kuhusu haki. Kadiri ulimwengu
unavyokuwa mgumu zaidi, ndivyo dhamira yetu ya kimaadili inavyopaswa kuwa
thabiti zaidi. Ninaamini Regan angekubaliana na kauli hiyo.
Hata hivyo, katika kuandika kitini kinachoitwa “Falsafa ya Haki za
Wanyama” hakumaanishi kwamba kazi ya Regan ni kamilifu au kwamba inaweza
kutumika bila dosari katika kila wakati na kwa kila hali. Maswali muhimu ya
kimaadili bado yapo. Kwa mfano, Regan asingekubaliana na Sheria ya Ustawi wa
Wanyama ya Sweden ya mwaka 1988, ambayo ilijaribu kupunguza kwa kiasi kikubwa
mateso katika ufugaji wa viwandani wa nguruwe pamoja na mageuzi mengine. Kabla
ya sheria hiyo, nguruwe jike hawakuwa wakifungiwa ili kulazimishwa kunyonyesha
watoto wao. Lakini sheria mpya ilihitaji kwamba nguruwe wote wawe na uhuru wa
kutembea badala ya kufungiwa kwenye vizimba vidogo, wapate majani na malazi
yanayofaa, wafugwe kwa makundi badala ya kutengwa, na pia ikakataza kukatwa
mikia na meno yao, ingawa utaratibu wa kuwahasi uliendelea kuruhusiwa. Hatua
hizi ziliondoa mateso makubwa kwa wanyama. Ni kweli kwamba Sweden haikupiga
marufuku kabisa ufugaji wa viwandani. Lakini je, mateso na vifo vya wanyama
nchini humo visingepaswa kushughulikiwa kwa namna hiyo, hata kama sheria hiyo
ilikuwa na mapungufu? Kwa ujumla, katika mifumo ya ufugaji wa viwandani, vifo
vya wanyama ni vingi zaidi. Viwango vya vifo vinaweza kufikia asilimia 15 huku
faida za kiuchumi zikiendelea kuongezeka. Tunaweza kuendelea kushikilia lengo
la kuanzisha haki za wanyama hadi siku ambayo dunia itakapokuwa tayari kwa hali
hiyo. Kwa sasa, ni jambo jema kwa “wale wanyama” wenye bahati wanaolindwa
katika makazi ya wanaharakati na vituo vya kuhifadhi wanyama, ambapo wanaishi
chini ya ulinzi wa misingi ya haki za wanyama. Lakini ni jambo la kusikitisha
kwa “wale wanyama” wasiokuwa na bahati wanaoteseka katika mazingira ya kikatili
ya ufugaji wa viwandani.
Katika kitini hiki, Regan anazungumzia umuhimu wa huruma, uwezo wa
kujihusisha na hisia za mwingine, na upole. Hata hivyo, kitabu chake The Case for Animal Rights (Hoja ya
Kutetea Haki za Wanyama) kinaakisi zaidi kauli nyingine inayopatikana pia katika kitini hiki: “Falsafa
ya haki za wanyama inahitaji tu: kwamba mantiki hiyo iheshimiwe.” Katika kazi
yake kuu, Regan hatoi uzito mkubwa kwa maadili ya kujali (care), jambo
ambalo limekosolewa na baadhi ya wanafalsafa wa kike (feminist philosophers).
Inawezekana mtu akakubaliana kwamba hoja za Regan zinaendana kikamilifu na mantiki, lakini wakati huo huo asiwe na
hisia zozote za kuwajali wanyama. Hali hiyo ingewanufaisha wanyama kwa kiwango
kidogo sana, au hata kutowanufaisha kabisa. Kwa upande mwingine, maadili
yanayojengwa juu ya huruma pekee nayo yana matatizo yake. Ikiwa unamwonea
huruma mtu mwingine—dhana ambayo ni msingi muhimu katika maadili ya kujali (care
ethics)—je, hilo lina thamani gani ikiwa mtu huyo mwenyewe ni fisadi au
mkatili? Kwa hiyo, mawazo yanayotegemea mantiki pekee na yale yanayotegemea
hisia pekee yote yanaweza kuzaa matatizo ya kimaadili. Swali linalobaki ni
hili: Je, tunaweza kujenga falsafa moja inayounganisha kwa usawa mantiki na
huruma?
Swali lingine muhimu ni: Ni wanyama gani wanapaswa kujumuishwa katika
haki za wanyama? Kwa suala hili, Regan anastahili pongezi nyingi. Anaonyesha
busara kwa kutetea haki za mbwa, lakini si haki za viumbe rahisi sana kama
amoeba. Hata hivyo, anasisitiza kwa uangalifu kwamba hata maumivu ya viumbe
kama konokono wasiokuwa na magamba (slugs) yanapaswa kuzingatiwa. Katika kitabu chake, Regan anafanya juhudi
kubwa kutetea msimamo wake kuhusu ni wanyama gani wanaostahili hadhi ya
kimaadili. Anawaita viumbe hao “subjects-of-a-life”, aani, viumbe ambao
ni wahusika wa maisha (wenye uzoefu
wa ulimwengu wao na ambao maisha yao yana umuhimu kwao binafsi). Hata hivyo,
bado maswali muhimu hubakia na ya kujiuliza. Lakini je, si jambo la kawaida
katika falsafa kwamba kila jibu hufungua nafasi ya kuuliza maswali mapya? Kwa
hiyo, tuendelee kuchunguza maswali haya kwa kina, huku tukiwatazama wanyama kwa
kuzingatia kile ambacho Regan alikiita kwa uzuri sana “kanuni ya heshima” (the
respect principle) katika kitabu chake cha The Case for Animal Rights (Hoja ya Kutetea Haki za Wanyama) …
Dk. David
Sztybel
Maberly,
Ontario, Canada
Januari 2026
Swahili Kiswahili